Naanza alifu, kumwomba Qudusi, Ilahi Jalali
Pili naturufu, nijuze insi, mada kukabili
Japo ni dhaifu, kamwe hakughasi, wala hakufeli
Nawataarifu, habari fususi, njoo musikili
Jina ni ufafu, ujue nususi, ya kwako usuli
Hujenga uswafu, kisha kutanisi, chimbuko la kweli
Wapata angafu, bada kudarisi, wepuke kisuli
Nawataarifu, habari fususi, njoo musikili
Hupa utukufu, majina halisi kawa ja asali
Huwishi kusifu, sifa ziso hasi, kujua asili
Huwi mdhaifu, kipata nemsi, ya kwenu famili
Nawataarifu, habari fususi, njoo musikili
Waza maradufu, bila ya nemsi, ngekuwaje hali?
Ngejua yusufu, au mwanamisi, au kina Ali?
Jina ni nadhifu, huleta ukwasi, tele `lokamili
Nawataarifu, habari fususi, njoo musikili
Hukupa ongofu, kujua upesi ya kwako asili
Hukutoka hofu, kadumu muhtasi, kaisha madhili
Jina ni ja dafu, utamu halisi, uso mushkeli
Nawataarifu, habari fususi, njoo musikili
Jina ni `tukufu, fahari wahisi, wajona jalili
Watu tastahifu, uwepuke msi, wewe kukujali
Jina si upofu, wala si kakasi,`tambulisho kweli
Nawataarifu, habari fususi, njoo musikili.
This poem was published in the 14th Issue of PoeticAfrica magazine.
Please click here to download.
More Poems:
Kabla Ya Kudijitika – Ijeiza Halima Kimani (Kenya)
Baby Alert – Chekete Christasia (Malawi)
Unfaded Portraits – Kaliu Prince (Malawi)
Echoes – Chukwuemeka V Chiamaka (Nigeria)
Ama Kweli Napendwa – Rajab Mulhat (Kenya)