Wino wangu nautua, ya uhondo kutongoa,
Ya moyoni kuyatua, na adili kuongoa,
Ya mekoni kufutua, yalo fiche kuzongoa,
Mlo wa nina sifia, metukuza ukubwani.
Nina hazina sifia, vya asili hifadhia,
Mafiga walitumia, sima bora andalia,
Mbaazi furahia, nazi tui miminia,
Mlo wa nina sifia, metukuza ukubwani.
Sijataja na muhogo, seredani wapikia,
Kweli wewe ni kigogo, nsi wote wafikia,
Tumboni hamna zogo, mwilini shabikia,
Mlo wa nina sifia, metukuza ukubwani.
Viazi vitamu raha, uji tamu ongezea,
Badani yawa fasaha, ‘zuri siha tazoea,
Hutokuwa wa mzaha, kazini tabobea,
Mlo wa nina sifia, metukuza ukubwani.
Kayani mna mchicha, na maziwa yalochacha,
Ni uhondo sitoficha, mezani ‘we hutoacha,
‘Somoni tawa galacha, tampiku wako pacha,
Mlo wa nina sifia, metukuza ukubwani.
Kadi tama tamatia, langu jamvi nalikunja,
Kaya mie napitia, ya upishi keshachanja,
Ya mekoni zingatia, sidhani kawa mjanja,
Mlo wa nina sifia, metukuza ukubwani.
This poem was published in the 10th Issue of PoeticAfrica magazine.
Please click here to download.
More Poems:
Kaibwaga Etu Mila na Kimani Halima (Kenya)
Soliloque – Mayssa Boulmaali (Algérie)