Elizabeth: …Mambo!
Nina hamu ya kusikia mengi kuhusu wewe Kristie.
Tumeona kazi yako kama mhariri wa jarida la kifasihi, tumesikia pia jina lako katika jamii ya uandishi na inastaajabisha kufahamu pia unafanya unachofanya kama mshairi. Kristie, nawiwa kufahamu zaidi, wewe ni nani nje ya kuwa mshairi?
Kristie: Asante sana. Nje ya kuwa mshairi, mimi ni mwandishi wa hadithi pia. Ila kwa taaluma nimesomea fani ya usanifu majengo katika ngazi ya shahada, na baada ya masomo yangu nilijaliwa nafasi ya kufanya kazi kama msaidizi wa msanifu majengo. Mbali na hapo, mimi ni mpenzi wa sanaa kwa ujumla. Iwe ni nyimbo, maigizo, uchoraji, ufinyanzi, ninafurahia sana kazi mbalimbali za sanaa. Vilevile mimi ni binti na ni dada katika familia ya Habakuki Lwendo, kitu ambacho ninakihesabu kuwa baraka sana.
Lisez – Une conversation avec Eloga Arsène
Swali la kizushi; Ni nani katika maisha halisi ulimfanya kuwa mhusika kwenye shairi lako?
Kristie: Mbali na mimi mwenyewe kuwa mhusika wa mashairi yangu, nimeshawahi kuandika kuhusu baba yangu na dada yangu pia.
Naam, inavutia sana. Ni dhamira gani zimepelekea uandike shairi lako?
Kristie: Nimeandika kuhusu Upendo, Maumivu, Kifo, na nyingine nyingi.
Ingetokea ukawa mwili wa mshairi fulani walau kwa siku moja tu, ungekuwa mwili wa nani?
Kristie: Swali gumu! Kuna washairi nguli wengi sana ningependa kupata nafasi ya kuwafahamu zaidi. Nadhani kwa Tanzania ni Shaaban Robert. Kimataifa, William Blake au hata Emily Dickinson. Ninapenda sana upekee katika uandishi wao.
Naomba kufahamu kuhusu uhusiano wako na ushairi; ulianza vipi, umekuwa mshairi kwa muda gani sasa, je uliwahi kukata tamaa, kwanini bado unatunga mashairi?
Kristie: Nilifahamu kusoma nikiwa mdogo sana, na nyumbani kulikua na vitabu vingi vya ushairi kwa sababu kaka yangu mkubwa alikua anasoma ushairi kama sehemu ya somo la Kiswahili shuleni. Nilikua navutiwa sana na mpangilio wa maneno katika ushairi, hivyo kwa sehemu kubwa sana vitabu hivyo vya kaka yangu vilikua vitabu vyangu pendwa pia. Nadhani mara ya kwanza kujaribu kuandika shairi langu mwenyewe nilikua nina umri wa miaka tisa, na baada ya hapo niliendelea kuandika japo haikua mara kwa mara. Mwaka 2017 nilijiunga na kikundi kimoja cha waandishi wa ushairi, na hii ndio ilinipa chachu hasa ya kuamua kufanya ushairi kuwa kitu endelevu kwenye maisha yangu. Niwe mkweli; sijawahi kukata tamaa katika uandishi! Na kitu kinachonifanya niendelee kutunga mashairi ni kwa sababu yamekua sehemu ya maisha yangu sasa. Yananisaidia kuelewa mambo mengi sana, hasa mawazo yangu binafsi na mitazamo yangu juu ya mambo mbalimbali. Kwa kiasi fulani, ushairi ni namna yangu ya kufikiri na kutathmini mambo.
Read – A Chat with Benny Wanjohi
Swadakta! Tupeleke kidogo katika maktaba yako ya mashairi: Yapi ni mashairi yako 10 pendwa? Matano ya kiswahili na matano ya lugha nyingine, sivyo?
Kristie: 1. Kama mnataka mali.
Kwa bahati mbaya sijawahi kufahamu mtunzi ni nani, ninakumbuka lilikua shairi pendwa sana tulipokua shule ya msingi.
- Samaki mekasirika.
- Kapatikana- Mtunzi ni Dotto Rangimoto.
- Dunia njema – Mtunzi ni Shaaban Robert.
- Diwani ya mloka. Yote! – Mtunzi ni Charles Mloka.
Mashairi ya kiingereza ninayoyapenda sana ni;
- Tyger, limeandikwa na William Blake.
- A poison tree, limeandikwa na William Blake.
- Because I could not stop for death, limeandikwa na Emily Dickinson
- When a boy tells you he loves you, limeandikwa na Edwin Bodney.
- Kitabu chote cha LONE, kimeandikwa na Anthony Onugba.
Ni shairi lipi linabeba hisia zako zaidi? Kwanini?
Kristie: Siwezi kuchagua moja. Kila shairi lina upekee wake, na moyo hutafsiri sanaa kulingana na wakati. Hivyo chaguo langu hubadilika mara kwa mara.
Je, shairi lako limewahi kuathiri afya yako ya akili?
Kristie: Hapana.
Unawaambia nini washairi ambao hutumia mashairi yao kuelezea hisia zao?
Kristie: Mbali ya kuelimisha, kuonya pamoja na kuburudisha, naamini uandishi ni tiba pia. Hivyo waendelee kutumia sanaa kuelezea hisia zao.
Read about – Nathaniel Z Mpofu – Multi-Award-Winning Zimbabwean Author
Ukipata fursa ya kuzungumza na waandishi wote barani Afrika, utawaambia nini?
Kristie: Wasiache kuandika. Waandike kila wanachoweza kuandika, kwa manufaa yao binafsi, ya kizazi hiki, na vizazi vijavyo.
Tuwe wanasiasa kidogo! Kwako ipi ni Ndoto ya Kiafrika kwa waandishi wa bara hili?
Kristie: Kusikika, kusikilizana na kuwa na umoja.
Tunaweza kupata wapi kazi zako baada ya mazungumzo haya?
Kristie: Kwa sasa, bado sijachapisha kitabu. Mungu akijalia nitachapisha hivi karibuni.
Asante sana Kristie kwa kuzungumza nasi. Ina maana kubwa sana. Ninashukuru sana kwa kupata wasaa huu.
Kristie: Mimi pia nimefurahia mahojiano haya.
Ahaa, basi jamani, tafadhali mfuate mgeni wetu Kristie katika:
Instagram: @kristiehabakuki
Twitter: @MutuMuandishi
This chat was published in the 7th Issue of PoeticAfrica magazine.
Please click here to download.
This Magazine is published by a team of professionals and downloadable for free. If you would like to support our work, please buy us coffee – https://www.buymeacoffee.com/wsamagazine