Vumbi la mahangaiko, na kelele za uchovu
Hunitia hamaniko, kuzidi ukakamavu
Leo niko kesho siko, mambo yataka utuvu
Siku huanza, kwa makelele na vishindo
Dunia ni mzunguko, haitaki udumavu
Tete wademao koko, huchomwa wawe majivu
Imara kama mikoko, huwalinda zao mbavu
Siku huanza, kwa harubu ya uwindo
Zitakuenea mboko, zivunje chako kidevu
Wakukimbie wenzako, walo na choyo na wivu
Dunia ya masumbuko, hutuvuta kama wavu
Siku huanza, kwa midomo ya uvundo
Afrika ndipo tulipo, nisikize kwa utuvu
Kwa kutofuata miko, kutwa tunashika shavu
Ama hili sikitiko, hututia udumavu
Siku huanza, kwa riziki ya mgando
Silaha za milipuko, zinoua usikivu
Zinoharibu masoko, ya kunde na ndizi mbivu
Zimetupwaya mbeleko, nyoyo zimejaa kovu
Siku huanza, kwa tabu na nyingi nyodo
Karafuu na Choroko, tele zimejaa kuvu
Wa kuziuza hawako, wamebakia mafuvu
Vita ni letu anguko, kisha twaitwa wavivu
Siku huanza, taratibu wake mwendo
Kaditama sikitiko, ndimi askari shupavu
Sipajui niendako, naushinda ulegevu
Afrika yangu na yako, tuwashinde waonevu
Siku huanza, kwa tamaa zilo kando.
This poem was published in the 7th Issue of PoeticAfrica magazine.
Please click here to download.
Read – Aumwapo – Mfaume Hamisi (Tanzania)
Read – Time is Now – Nakut Janet (Kenya)
This Magazine is published by a team of professionals and downloadable for free. If you would like to support our work, please buy us coffee – https://www.buymeacoffee.com/wsamagazine