Naanza hino nudhuma, Namweka mbele karima
Kwangu kanipa uzima, Na siwezi kulalama
Leo takuwa mtema, Yalo moyoni kusema
Mti kunyauka shina, Sio kufa kwa matawi
Hautokosa uzima, Mti ulo na matawi
Shinale ukikatama, Ukuni kamwe hauwi
Mizizi itashikama, Japo maji hayatiwi
Mti kunyauka shina, Sio kufa kwa matawi
Hakika ninaungama, Kwetu yali mambo mawi
Lipofa baba na mama, Vurugu ilisheheni
Ufungu wetu lizama, Tukawa hatwelewani
Mti kunyauka shina, Sio kufa kwa matawi
Mimi naitwa Sogoli, Nilirithi babu Tale
Zapendwa zangu amali, Kutokako enzi zile
Japo leo hatukuli, Pamoja ilivyo kale
Hakika kufa kwa shina, Sio mwisho wa matawi
Bado waweza chipuka, Mti shina likikatwa
Hata sasa napendeka, Kwa sifaze nileitwa
Mambo yake lichekeka, Usiku mchana kutwa
Kweli kukufa kwa shina, Sio mwisho wa matawi
Sifaze za kupendana, Na watu kuunganisha
Babu Tale alifana, Kila siku za maisha
Ona leo twaungana, Kisa alisababisha
Na’mini kufa kwa shina, Sio mwisho wa matawi.
This poem was published in the 14th Issue of PoeticAfrica magazine.
Please click here to download.
More Poems:
Fu-Su-Li – Rashid Athuman (Kenya)
Kabla Ya Kudijitika – Ijeiza Halima Kimani (Kenya)
Baby Alert – Chekete Christasia (Malawi)
Unfaded Portraits – Kaliu Prince (Malawi)