Nikitazama dunia, moyoni nahuzunika,
Sina la kujivunia, hata kule Amerika,
Tena najihurumia, kwayo yanayotendeka.
Redio ‘kisikiliza, ni balaa na beluwa,
Televisheni chunguza, uonayo si muruwa,
Utu tumeupoteza, mwanadamu kapagawa.
Wakubwa wanasutana, mabavu kuoneshana,
Kisha wanatishiana, wao hata kuuana,
Wa kuzuia hakuna, sisi sauti hatuna.
Uringoni kuna ndondi, wenye nguvu wadundana,
Wameunda na makundi, misuli kutunishana,
Mnyonge hana ushindi, ye’ watamchanachana.
Wanatamba wenye shibe, watupigishe miayo,
Hawasemwi kwa ubabe, wanafanya wapendayo,
Bora yangekuwa ngebe, tusingevunjka moyo.
Dunia yawayawaya, hao wameichafua,
Na hata kule Ulaya, salama imepungua,
Binadamu bila haya, wengine hujilipua.
Hofu iko pande zote, dunia ipo tamati,
Kama kwetu hali tete, yatungojea mauti,
Mola katutema mate, waja hatuna bahati.
This poem was published in the 7th Issue of PoeticAfrica magazine.
Please click here to download.
Read – Halibari – Amri Rajabu Abdalah (Tanzania)
This Magazine is published by a team of professionals and downloadable for free. If you would like to support our work, please buy us coffee – https://www.buymeacoffee.com/wsamagazine